KUSENGENYA
📚📚 *KUSEMGENYA:" Ni Kumtaja Mtu Kwa Jambo Analolichukia* 📚📚
Haifai kumsema mtu hata ikiwa mtu huyo ana sifa mbaya unayoitaja madamu unaitaja nyuma yake basi huwa ni kusengenya kama alivyosema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alaihi wa aalihi wa sallam). Basi seuze iwe ni kumsengenya mtu kwa aibu asiyokuwa nayo au kumtolea aibu zake, au kumzulia kwa mabaya asiyokuwa nayo?
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَال:
أَتَدْرُونَ مَا الْغِيبَةُ ؟ قَالُوا : اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَعْلَمُ ، قَالَ : ذِكْرُكَ أَخَاكَ بِمَا يَكْرَهُ ،
قِيلَ : أَفَرَأَيْتَ إِنْ كَانَ فِي أَخِي مَا أَقُولُ؟
قَالَ :إِنْ كَانَ فِيهِ مَا تَقُولُ فَقَدِ اغْتَبْتَهُ ، وَإِنْ لَمْ يَكُنْ فِيهِ فَقَدْ بَهَتَّهُ
أخرجه مسلم
Kutoka kwa Abu Hurairah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba aliuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu Alaihi wa aalihi wa sallam):
"Je mnajua maana ya Ghiybah (kusengenya)?
Wakasema:
"Allaah na Rasuli Wake wanajua."
Akasema:
"Ni kumtaja ndugu yako kwa jambo analolichukia"
Akaulizwa:
"Hebu nieleze, iwapo ndugu yangu anayo yale niyasemayo?"
Akasema:
"Ikiwa analo hilo usemalo basi umeshamsengenya, na ikiwa hana hilo usemalo basi umeshamzushia uongo"
{Muslim}
Kwa hivyo ukimsema mtu:
"Ni mbishani", "Hajui kusema na watu", "Anajiona", "Amependa kukasirika", "Uzee unamsumbua"
Huyo mtu akiyasikia akachukia na asifurahie ujue umemsengenya.
Je, ni wangapi kati yetu kila siku tunasengenya na ni mara ngapi tunasengenya kwa siku?
*Enyi Wasengenyaji! Mjue Kila Mnaposengenya Mnajichumia Madhambi Na Kupoteza Mema Yenu Mliyoyatenda*
Bila shaka kusengenya mtu mwingine itakuwa ni kujichumia dhambi ambayo mtu huadhibiwa na vile vile ni kupoteza mema yako unayofanya kuwa anapewa huyo unayemsengenya. Mwenye kuzidi kusengenya huendelea kupoteza thawabu zake hadi anapokuwa hana kilichobakia katika mema yake, hapo tena hujazwa madhambi ya wale aliowasengenya.
Kusengenya hakika ni hatari mno kwa Muislamu kwani kusengenya zinamharibia mtu ‘amali zake na hatimaye akute patupu katika mizani yake ya amali njema Siku ya Kiyama. Hatari hii ni kwa yeyote yule hata kama mtu ni mswalihina au ni mtendaji wema kwa wingi!
Tumeonywa sana uovu huu katika Qur-aan na Sunnah.
وَلَا يَغْتَب بَّعْضُكُم بَعْضًا ۚ أَيُحِبُّ أَحَدُكُمْ أَن يَأْكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوهُ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ ٌ﴿١٢﴾
12. ...na wala wasisengenyane baadhi yenu wengineo. Je, anapenda mmoja wenu kwamba ale nyama ya nduguye aliyekufa?
Basi mmelichukia hilo! Na mcheni Allaah!...
{Al-Hujuraat: 12}
Baadhi ya hizo adhabu za Aakhirah ikiwemo adhabu ya kusengenya alikwishaziona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu Alaihi wa aalihi wa sallam) alipokwenda Israa wal Mi'raaj kama ilivyotajwa katika Hadithi ifuatayo:
عن أنس قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم:
لما عُرِجَ بي مررتُ بقومٍ لهم أظفارٌ من نُحاسٍ يخْمِشون وجوهَهم وصدورَهم، فقلتُ: من هؤلاء يا جبريلُ ؟
قال: هؤلاء الذين يأكلون لحومِ الناسِ ، ويقعون في أعراضِهم.
Kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu Alaihi wa aalihi wa sallam) amesema:
Nilipopandishwa mbinguni (Siku ya Israa na Mi’raaj) nilipita kwa watu ambao walikuwa wana kucha za shaba nyeupe wakijichana nyuso zao na vifua vyao.
Nikauliza: "Nani hawa ewe Jibriyl?"
Akasema: "Hawa ni watu ambao wamekula nyama za binaadamu na kuwavunjia heshima zao"
{Abu Dawud}
*Wanaosengenya Wenzao Wachunge Amali Zao Njema Zisije Zikafilisika Siku Ya Kiyama Kwa Kupewa Walio Wasengenya Wakiishiwa Na Mema Wapewe Madhambi Zao Waliowasengenya*
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: أَتَدْرُونَ مَا الْمُفْلِسُ؟
قَالُوا: الْمُفْلِسُ فِينَا مَنْ لاَ دِرْهَمَ لَهُ وَلاَ مَتَاعَ .
فَقَالَ: إِنَّ الْمُفْلِسَ مِنْ أُمَّتِي يَأْتِي يَوْمَ الْقِيَامَةِ بِصَلاَةٍ وَصِيَامٍ وَزَكَاةٍ وَيَأْتِي قَدْ شَتَمَ هَذَا وَقَذَفَ هَذَا وَأَكَلَ مَالَ هَذَا وَسَفَكَ دَمَ هَذَا وَضَرَبَ هَذَا فَيُعْطَى هَذَا مِنْ حَسَنَاتِهِ وَهَذَا مِنْ حَسَنَاتِهِ فَإِنْ فَنِيَتْ حَسَنَاتُهُ قَبْلَ أَنْ يُقْضَى مَا عَلَيْهِ أُخِذَ مِنْ خَطَايَاهُمْ فَطُرِحَتْ عَلَيْهِ ثُمَّ طُرِحَ فِي النَّارِ
مسلم
Kutoka kwa Abu Hurairah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
"Je, Mnamjua muflis?"
Wakasema: “Muflis kwetu sisi ni yule miongoni mwetu asiyekuwa na dirhamu (pesa) wala vyenye kumnufaisha yeye hapa duniani”.
Akasema (صلى الله عليه وآله وسلم): "Hakika muflis katika Ummah wangu ni yule atakayekuja Siku ya Kiyama na Swalaah, Swiyaam, na Zakaah, lakini amemtusi huyu, kumsingizia huyu mwingine kuwa amezini, amekula mali ya huyu, amemwaga damu ya mwingine na kumpiga mwengine. Thawabu zake zitapatiwa huyu na yule mpaka zimalizike. Na zinapokwisha basi madhambi ya hao atabandikwa nayo, hivyo kuingizwa Motoni"
{Muslim}
Ukweli ni kuwa wengi wetu tumependa sana kuwasengenya watu, hata kuliko tunavyokunywa maji na kula kwa siku. Kila wakati twasengenya; tukiongea kwa simu, tukikaa, tukitembea, tukila twasengenya.
Uamuzi ni wetu, aidha tuchunge amali zetu njema kwa kuacha kusengenya na kuzidisha mema au tufilisishe amali zetu njema kwa kutoacha kusengenya na maasi.
Je wakati wa kubadilika na kuacha kusengenya na maasi haujafika?
📚📚📚📚📚📚📚📚📚📚
WASAMBAZAJI
QURAN NA SUNNAH BLOGGER
WHATSAPP NO +255713849566
TEMBLEA BLOGGER YETU KWA KUSOMA DARASA ZETU ZAIDI
http://qurannasunnahtz.blogspot.com/
No comments